NACTE YATOA UFAFAUNZI KUHUSU MAOMBI YA NAMBA YA UHAKIKI WA TUZO (AVN) KWA WAHITIMU WANAOTAKA KUJIUNGA NA ELIMU YA JUU
BARAZA la Taifa la Elimu ya
Ufundi( NACTE) limetoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya kuchelewa kupata
Namba ya Uhakiki wa Tuzo (AVN) yanayotolewa na baadhi ya wahitimu wa
ngazi ya stashahada hasa waliomaliza masomo katika mwaka wa masomo wa
2017/2018.
Mkuu wa Kitengo cha Udahili NACTE
Twaha A. Twaha, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam
leo tarehe 24 Agosti, 2018 kitendo cha vyuo na taasisi za elimu
kutowasilisha mapema matokeo halisi ya wahitimu kwenye baraza hilo,
kimepelekea wahitimu hao kukwama katika maombi ya AVN.
Twaha ameeleza kuwa, hakuna
mhitimu wa ngazi ya diploma anayeweza kujiunga na elimu ya juu bila ya
kuwa na AVN na kwamba wahitimu hao wanapaswa kuwa na vigezo stahiki
wakati wanapofanya maombi NACTE ili wapate namba hiyo itakayowawezesha
kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.
“Kumekuwepo na malalamiko ya
baadhi ya wahitimu wa ngazi ya stashahada na hasa waliomaliza masomo yao
kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi mwezi Julai, 2018. Baadhi ya
wahitimu hao mara tu baada ya kumaliza mitihani yao na kupatiwa matokeo
ya awali wamekuwa wakiomba AVN kwa kuambatanisha hati za matokeo ya
awali wakati vyuo na taasisi husika hazijawasilisha NAVTE matokeo halisi
yaliyoidhinishwa na mamlaka husika,” amesema Twaha na kuongeza.
“ Na pia uhakiki wa matokeo yao
haujakamilika kwenye mfumo wa uhakiki wa Tuzo wa Baraza. Ifahamike
kwamba hakuna mhitimu wa ngazi ya diploma anayeweza kujiunga na elimu ya
juu bila kuwa na AVN. Huu ni utaratibu uliowekwa na baraza ili
kurahisisha utambuzi wa tuzo za elimu na mafunzo ya ufundi stadi
nchini.”
Kufuatia malalamiko hayo, Twaha
amevitaka vyuo na taasisi za elimu kutoa matokeo ya wahitimu wao mapema
kwa ajili ya kuwarahisishia kupata Namba ya Uhakiki wa Tuzo (AVN)
itakayowawezesha kujiunga na elimu ya juu.
No comments