WAZIRI MKUU AMWAGIZA RPC SHINYANGA AWAKAMATE VIONGOZI TISA WA AMCOS YA USHETU
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,
Simon Haule awakamate viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa
upotevu wa dola za marekani 21,000 za chama hicho.
"Wabebe
hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete
hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani,"
amesema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 16, 2018) wakati
akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa
katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambao alienda kuzindua
mpango wa Ushirika Afya na NHIF.
Waziri
Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuwaita viongozi wa chama cha
Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa
kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.
Kamanda
Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti, Bw. Shilinde
Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Bw. Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe
saba wa bodi ya chama hicho.
Akiwa
katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama
(KACU), Bw. Emmanuel Cherehani alisoma taarifa ya Chama na alipotaja bei
ya tumbaku kuwa ni nzuri, wananchi walimzomea kupinga kile
alichokisema. Bw. Cherehani alikuwa akitoa mafanikio ya chama hicho, na
kusema kuwa bei ya tumbaku ni nzuri.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba
alisema kuna tatizo katika uteuzi (grading) wa tumbaku kwani wakulima
wanalima tumbaku nzuri lakini katika upangaji bei, wanalipwa bei ndogo.
“Kuna wakulima wanakidai chama cha Mkombozi kiasi cha dola za Marekani
ambayo ni madai ya tumbaku waliyoiuza tangu mwaka 2014.”
Akizungumza
na wananchi hao, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kufufua ushirika
kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha ushirika
aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata
dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.”
“Tunataka
ushirika unaosimamiwa na viongozi waaminifu. Kwenye ushirika kuna fedha
na kuna mali za chama, kwa hiyo ni lazima tupate viongozi ambao ni
waaminifu,” amesema.
“Kwa
mfano, hapa Ulowa wakulima wamekuwa wakilalamikia kupewa bei ya chini
wakati wakati wao viongozi wanabeba kile cha juu na kuwaumiza wakulima.
Kiongozi wa KACU kasoma taarifa hapa mkaanza kuzomea, hiyo ni dalili
tosha kwamba kuna tatizo la msingi,” amesema.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa wakulima waachane na tabia ya kukopa
pembejeo na kufunga mikataba na makampuni ya ununuzi wa tumbaku na
badala yake wajiwekee akiba ili msimu wa kilimo ukianza wasirudie tena
kukopa.
“Gharama
za kulima ekari moja, kuweka dawa, palizi na kuchoma haizidi sh.
150,000. Wewe amua unataka kulima ekari ngapi, weka fedha zako kwenye
akaunti usubiri msimu ujao. Kwenye hii biashara ya tumbaku, ukitafuta
mikopo utabakia kuwa maskini kwa sababu huna nguvu ya kubishania bei.
Wenzenu wanaolima korosho, wameacha kukopa na bei mnazisikia kila mwaka
zinapanda,” amesema.
“Ukiwa
na mazao yako utaweza kubishana na mnunuzi. Tanzania bei ya tumbaku iko
chini sababu wakulima mmetufikisha hapo kwa kupitia mikopo na mikataba
na makampuni ya ununuzi. Kuanzia sasa badilikeni, ili muweze kuinua bei
ya zao hili muhimu, alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa Kijiji cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga wakati alipowasili kijijini hapo kuhututibia Mkutano wa hadhara na kuzindua Fao la Ushirika Afya ambalo litawazesha wanaushirika kunufaika na huduma za Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya, Julai 16, 2018 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. (kushoto) wakati alipokagua uuzaji wa tumbaku katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu, Julai 16, 2018. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeloeo ya Ushirika Nchini, Dkt. Titus Kamani Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kangeme kwenye Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Julai 16, 2018. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Fao la Ushirika Afya ambalo litawawezesha wanaushirika kunufaika na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwenye kijiji cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga Julai 16, 2018. Kushoto kwake ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, watatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Kong Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasha gari alilolizindua ambalo limenunuliwa na Halmashauri ya Ushetu kwa ajili ya Idara ya Kilimo ya Halmashauri hiyo , kwenye kijiji cha Kangeme Julai 16, 2018
No comments